Kuanzishwa kwa Mamlaka:

 Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma ilianzishwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 3 ya Mwaka 2001 ambapo baada ya Sheria hii kufutwa, Mamlaka iliendelezwa chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya Mwaka 2004 na kuhuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 baada ya ile Sheria Na. 21 ya Mwaka 2004 kufutwa.

Dhumuni hasa la kuanzishwa kwa Mamlaka hii ni kuwa na chombo mbadala cha kutatua migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma kwa muda mfupi zaidi tofauti na Mahakama za kawaida ili kutokuchelewesha utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Mamlaka hii pia husimamia utawala bora kupitia utatuzi wa migogoro inayowasilishwa mbele yake kwa kuhakikisha kuwa zabuni zinatolewa kwa wazabuni wenye sifa stahiki za kufanya kazi husika na hivyo kuwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zake katika ununuzi wa Umma.

Majukumu ya Mamlaka:-

  • Kupokea malalamiko na rufaa zitokanazo na  michakato ya ununuzi wa Umma;
  • Kufanya mapitio ya maamuzi ya Maafisa Masuuli kuhusiana na michakato ya ununuzi wa Umma;
  • Kufanya mapitio ya uamuzi uliofanywa na Mamlaka ya Uthibiti ya Ununuzi Umma kuhusu kuwafungia wazabuni (Blacklisting of tenderers);
  • Kuchukua hatua za kurekebisha pale inapoonekana kuna ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika michakato ya ununuzi.

Dira  

Kuwa chombo cha mfano kinachoheshimika kwa maamuzi yake yanayozingatia haki katika utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma.

 


Dhima

Kuchangia katika kukuza uchumi kwa kuimarisha uwajibikaji katika ununuzi wa Umma kwa kutoa maamuzi ya haki kwa muda stahiki.

 Katika kutekeleza jukumu lake la msingi la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma au kufungiwa kwa makampuni (blacklisting of Tenderers) Mamlaka huzingatia haki na usawa,  uadilifu, uwazi na uwajibikaji  na kutoa maamuzi kwa wakati.

 

 

MOTO: Kutoa Maamuzi ya Haki na Kwa Wakati